MENU

Where the world comes to study the Bible

5. Mafundisho Ya Biblia Juu Ya Utatu

Related Media

Sikuwa natarajia kuziona siku 45 zilizokuwa zinafuata. Kama ilivyo kwa familia za kijeshi kila mahali, nilikuwa nikitoka kwa ajili ya biashara ya Mjomba Sam kwa muda wa wiki sita, na nikiwa na mke kijana na watoto watatu wadogo nyumbani, ilikuwa sio mchezo. Kuna jambo moja katika safari hii ambalo lilikuwa rahisi—ni kwamba nilikuwa nakwenda kukaa na Mkristo katika chumba changu. Nilikuwa natarajia kuwa na ushirika wa Kikristo nikiwa na Mkristo mwenzangu, lakini hata hivyo nitaendelea kupata kelele za nyimbo za walevi wa awali niliokuwa nao.

Baada ya kumaliza shughuli zetu za siku ya kwanza, mimi na Bill tuliingia katika ushirika wetu wa kwanza siku ile usiku. Baada ya kujifunza kwa kama dakika tano hivi, niligundua jambo la ajabu sana—Bill alikuwa amefundishwa mafundisho potofu juu ya Utatu katika kanisa lake. Nilishangaa sana kwamba alikuwa kwenye kanisa la kiBaptist ambalo lilisifika sana kwa kuihubiri Biblia, kufanya kazi za Misioni na Uinjilisti. Nilijua kuwa alikuwa akihudhuria mafundisho ya Biblia katikati ya wiki pamoja na Jumapili asubuhi na jioni; kuhubiri usiku na shule ya Jumapili. Alikuwa ameokokea katika hili Kanisa miaka mitatu nyuma—ilikuwaje asijue mafundisho ya ki-orthodox juu ya Utatu?

Siku chache zilizofuata, nilimwonyesha kile Biblia inachofundisha kuhusu Mungu wa Utatu, na alikuja kuuona ukweli. Pia niligundua jinsi alivyokutana na huu mtazamo potofu alioupata kabla. Kwa miaka mitatu akiwa katika ushirika wa kujifunza katika kanisa hili kubwa, maarufu na linalosifika, la kiBaptisti, hakuwahi kusikia Utatu ukitajwa hata mara moja. Uelewa wake ulitokana na majibu yaliyokosewa kutoka kwa Mwalimu wake wakati Bill alipojaribu kuuliza kuhusu jambo hili kipekee. Katika siku zetu 45 za kukaa pamoja, tulishirikishana mambo mengi na niligundua kwamba kanisa hili “maarufu” lilisisitiza tu juu ya Yohana 3:16, zaka, mwenendo mzuri na kurudi kwa Yesu Kristo mara ya pili—ni mafundisho mazuri lakini hayajabeba kweli yote.

Katika historia yote ya kanisa, maadui wa Mungu wamekuwa wakishambulia mafundisho ya kiBiblia kuhusu Asili, na hasa Uungu wa Mwana wa Mungu. Somo tunalokwenda kugusa hapa ni miongoni mwa mambo yanayoshambuliwa sana (na pia yanayotetewa) katika mafundisho makuu ya Imani: Mungu ni mmoja katika Utatu ambaye anajidhihirisha kama Baba, Mwana, na Roho (nafsi tatu ambazo ni tofauti)—lakini bado ni katika Mungu mmoja. Hili linaitwa ni fundisho la UTATU tangu wakati wa kanisa la kwanza, lakini vita vilivyojitokeza katika kanisa la kwanza na mijadala ya kifalsafa kuhusu fundisho hili yamepindisha dhana kwamba fundisho la Utatu linaungwa mkono kwa nguvu na Maandiko Matakatifu, na limetokana na Maandiko.

Kauli rahisi ambayo tumeitoa imetokana na maneno ya kitaalam yanayoelezea kile Biblia inachofundisha kila mahali kuhusu somo hili. Hii siielewi hata kwa sekunde. Hata hivyo, naelewa vizuri sana kwamba Biblia inafundisha mambo haya, kwa hiyo nayaamini na kuyafundisha bila kujali kwamba nayaelewa vizuri au la. Kwa hiyo, mawazo ambayo tunatakiwa kuwa nayo wakati tunashughulika na fundisho la Utatu ni hili: AMINI KILE BIBLIA INACHOFUNDISHA NA USIJARIBU TU KUKIELEWA. Fikiri kuhusu suala hili—fundisho hili linazungumzia asili muhimu sana ya Mungu, tunawezaje kulielewa?

Kwa kweli, karibu kila kikundi chenye mafundisho potofu ambacho kimeponyoka kutoka kwenye imani ya Kiinjili ya Kikristo, ama kilianza na mtu mmoja akijaribu kuuelezea Utatu au mafundisho ambayo yanakaribiana sana na harakati za kikundi hicho. Tukianza na wapotoshaji ambao walikuwepo wakati mitume wakiwa hapa duniani, na kuendelea na vikundi vya imani potofu ambavyo viliibuka miaka ya 60 pamoja na wainjilisti wanaotembea siku za leo, kukataa, kupinga au kupotosha mafundisho juu ya Utatu limekuwa ni jambo la kawaida kwa karibu wote hao.

  • Leo Mashahidi wa Jehova na Kanisa la Njia wanaukataa Uungu wa Yesu na pia nafasi na Uungu wa Roho Mtakatifu.
  • Watu wa Mormons na Armstrong (wanaodai kuwa ni Kanisa la Mungu la Ulimwengu) wanaamini aina fulani ya miungu wengi.
  • Makanisa mengi ya kipentekoste wanaamini katika upotoshwaji wa Utatu ambao humfanya Mungu kuwa anajifanya kuwa kama watu tofauti kwa nyakati tofauti. Utasikia wakisema “Uungu Mmoja” au “Yesu Tu”. Hii inafanana na vikundi vilivyoibuka kama miaka 1500 iliyopita.
  • Mtazamo wa kanisa la Orthodox pamoja na makanisa yake ya Kiinjili, Wakatoliki wa Roma, wamekuwa wakikataa fundisho la Utatu ambalo lilitolewa kwa watakatifu (Yuda 3).

Katika kujadili fundisho hili muhimu, nitajaribu kuepuka maneno ya kitaalamu ya kiufundi, lakini nitajikita zaidi katika maneno rahisi ya Biblia. Kutokana na umuhimu mkubwa wa fundisho hili, na hitaji la kupitia misingi yote muhimu, nitakupa mistari mingi ya Biblia ili ujisomee mwenyewe.

Fundisho la Utatu lina vipengele vifuatavyo: (1) Kuna Mungu Mmoja tu wa Kweli (2) Kuna “nafsi” katika Mungu ambazo sio za kufikirika, kubuni au za muda. (3) Baba ni Mungu (4) Mwana ni Mungu (5) Roho Mtakatifu ni Mungu. Zinakuwa kama zile hisabati za ajabu ambazo nimejifunza na hazina maana halisi ya hesabu za kibinadamu: yaani 1 + 1 + 1 = 1 badala ya 3. Yaani hapo ni jumla ya tatu bado inakuwa moja na tunasema kuna “utatu” katika hiyo moja ambapo Biblia inajaribu kuionyesha bila kujaribu kuelezea.

Kuna Mungu Wa Kweli Mmoja Tu [Monotheism]

Maadui wengi wa Ukristo, wakiwemo Waislam, Wayahudi, na Wakengeufu wengine kama Mashahidi wa Jehova, wamedai kwamba Utatu ni upagani kwa sababu ni kuabudu zaidi ya “mungu” mmoja. Hata hivyo msingi wa mafundisho ya Utatu ni kwamba kuna Mungu Mmoja tu. Hii inafundishwa kwa msisitizo katika Agano Jipya na Agano la Kale. Kauli ya imani ya Isaraeli inasema “Sikia ee Israel, BWANA Mungu wetu ni BWANA mmoja.” (Kumb. 6:4). Yesu alipoulizwa, alisema zaidi ya mara moja kwamba hii ndio ilikuwa amri kuu kuliko zote (Marko 12:28-34).

Uwazi wa Umoja wa Mungu umeelezwa kwa kurudia sana katika Agano la Kale: “…hapana mungu mwingine ila mimi” (Kumb. 32:39); “…Mimi ni BWANA, wala Hapana mwingine.”(Isa. 45:18); “…kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. (Isa. 43:10). Vivyo hivyo, Agano Jipya linaeleza u-moja wa Mungu: “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja (1 Tim 2:5); “…na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo, uliyemtuma…” (Yn. 17:3).

Katika Agano la Kale, Mungu alijitangaza kwa kutumia majina mengi, kila moja likielezea sifa yake, lakini jina lake la sifa alilotumia kufanya agano na watu lilikuwa ni YHWH au Yawe kulingana na matumizi ya lugha. Jina hili ndilo lililotafsiriwa kuwa Yehova. Tafsiri nyingi ndizo zilizoleta jina BWANA au MUNGU, kwa kuandika herufi zote kuwa kubwa. Yehova alitafsiri jina lake kwa Musa katika Kutoka 3:14: MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu.” “MIMI NIKO AMBAYE NIKO” … Yehova hana kitu au mtu anayemdai katika kuishi kwake—Yeye anaishi na yuko peke yake, Mungu Mmoja wa Kweli.

Wingi: Katika Mungu Mmoja Wa Kweli Kuna Wingi Wa Nafsi

Katika matamko yenye nguvu Biblia inayoyatoa juu ya Mungu mmoja, hii ndiyo kauli yenye utata. Hata hivyo Biblia iko wazi juu ya wazo hili. Kwa kweli iko wazi kabisa kuwa kuna Mungu Mmoja. Hata hivyo, kuna wingi wa nafsi katika “u-tatu” kuhusu Mungu ambao Biblia inauelezea, ambao hatuwezi kuuelezea kwa namna za kibinadamu kwa mitazamo wa Umoja wake. Kwanza kuna maneno na majina ya wingi ambayo yanatumika kwa Mungu. Neno maarufu zaidi katika Biblia ni neno la Kiebrania Elohim. Vikundi kengeufu vimejaribu kutunga sababu za kwa nini Biblia inatumia wingi kumwelezea Mungu Mmoja, lakini maneno machache kutoka kwa mtakatifu wa zamani aitwaye John Gill yatawafanya watulie:

“Sasa Musa angaliweza kutumia majina mengine ya Mungu, katika kuelezea uumbaji, kama jina lake la Yehova, kwa kuwa ndilo ambalo Mungu alikuwa amejifunua nalo kwake, na kwa watu wa Israel; au Eloah, ambalo ni jina la Umoja la Elohim, ambalo alilitumia (Kumb. 32:15-16) na pia katika kitabu cha Ayubu mara nyingi; kwa hiyo lilikuwa siyo hitaji la maneno ya Umoja ya Mungu, wala udhaifu wa lugha ya Kiebrania iliyomlazimisha kutumia neno la wingi; ndivyo alivyochagua na kuipangilia…” (Body of Divinity, Kit. 1 uk. 187-188).

Maneno mengine yaliyoko katika hali ya wingi yaliyotumika kwa Mungu katika Agano la Kale ni pamoja na panim (sawa na prosopa, kumaanisha “nyuso,” “watu,” au “uwepo,”) ambalo linapatikana katika Kutoka 33:14-15, Zaburi 27:8-9, na Kumb. 4:37; neno la Kiebrania la Mtengenezaji au Muumba katika Ayubu 35:10, Zab 149:2, na Isaya 54:5 ni wingi, Watengenezaji; katika Mhu. 12:1, neno la Kiebrania ni Waumbaji. Mungu pia ameelezewa kwa neno la wingi, kama “…na tumfanye mtu kwa mfano wetu.”(Mwa. 1:26), angalia pia Mwanzo 11:6-8 na Isaya 6:8. Hatimaye katika Isa. 48:16-17 ni Tamko ambalo, likisomwa katika mwanga wa Agano Jipya, ni Tamko la Utatu kama lilivyo mahali popote katika Biblia, kama Bwana Mungu (Adonai Yehova) Roho. Na Mkombozi yote yametajwa katika mazingira yale yale ya watu tofauti.

Bila shaka kuna Maandiko mengi katika Agano Jipya yanayoongelea Baba, Mwana na Roho Mtakatifu katika muktadha uleule, na kwa mtazamo wa wazi unaozitofautisha. Katika Yohana 14 hadi 16, kuna rejea zinazojirudia kwa kutoa tofauti hizi. Iliyoko wazi zaidi ni ile ya Ubatizo wa Yesu katika Mathayo 3:16-17, ambapo tunaisikia sauti ya Baba, angalia Roho alishuka kwa mfano wa hua, na ona pia kwamba Mwana amesimama pale katika maji.

Baba Ni Mungu

Hii haingehitaji kusemwa, lakini kwa sababu ya wale wanaokataa uhalali wa nafsi ya kwanza ya Utatu, tunatamka kwamba (a) Yesu mara nyingi anaitwa ni Mwana wa Mungu, kwa hiyo Mungu ni Baba, na Baba ni Mungu. (b) Hakuna Maandiko yanayoonyesha hata kudokeza kwamba Baba anakoma kuwa Nafsi ya tofauti. (c) Kuna Maandiko mengi ambayo yanathibitisha kwamba kuna tofauti kati ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tatizo hapa, kama lilivyodokezwa na Gregory A. Boyd katika kitabu chake, Oneness Pentecostals and the Trinity, ni kwamba, wakati watu wanapoyasoma Maandiko wakiwa na mawazo mgando (kama vile mafundisho potofu kwamba hakuna tofauti kati ya Baba na Mwana), huviona vitu katika Biblia ambavyo havipo!

Ugumu mwingine (ambao ni maarufu kwa mapokeo yanaodai kuwa Yesu si Mungu) ni kwamba watu wengi wanashindwa kuelewa uhusiano kati ya Baba na Yesu Kristo. Sababu ya kushindwa kuelewa huku ni kwamba wanashikilia maneno yaliyosemwa na Yesu au juu ya Yesu wakati alipokuwa akiteswa hapa duniani. Uhusiano wa milele kati ya Baba na Mwana ni wa Usawa (Yohana 17:1 – 5, angalia anavyosemakwa Baba, na Ebr. 1:1-14, ambapo Baba anaagiza malaika wamsujudie. Kauli kama “…Baba yangu ni mkuu kuliko mimi.” (Yohana 14:28) inapaswa ieleweke katika mwanga wa kusudi lake katika huduma yake hapa duniani. Katika Waebrania, baada ya kuanza kwa kuangalia hali ya kuinuliwa na uungu wa Mwana (1:1-14) mtume anasema, “lakini tunamwona Yesu ambaye alifanywa mdogo punde kuliko malaika kwa ajili ya mateso ya mauti…”( angalia pia Flp. 2:5-11). Yesu alikuja duniani kukamilisha ukombozi wa milele. Uungu wake, ambao ni wa muhimu, ulifichwa katika mwili. Lakini kama jambo letu la pili linavyoeleza:

Yesu Kristo Ni Mungu

Sio tu kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, Yeye ni Mungu-Mwana. Hili ndilo fundisho la msingi la Ukristo—Yesu Mwenyewe alisema “…Msipoamini kwamba Mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.”(Yn. 8:24) Haya siyo tu mafundisho ya uchunguzi au falsafa—kama Mungu mwenyewe hatatukomboa hatutaweza kukombolewa (angalia Zab. 49:7, 15)! Kwanza tunajua kuwa Yeye ni Mungu kwa sababu anaitwa Mungu (Yn. 1:1). Ni kweli, katika Yn. 20:28, ambapo Thomaso anamwita Yesu “Bwana wangu na Mungu wangu…” kwa kiyunani inasomeka “…Bwana wa mimi na Mungu wa mimi.” Waebrania 1:4-14 ni kifungu muhimu sana cha maandiko, kwani manabii wa Agano la Kale wananukuliwa kuonyesha (1) Mungu anamwita Yesu Mwanawe, (2) Anawaambia malaika wamwabudu Kristo, heshima ambayo huwa anapewa Yehova pekee (Isa. 42:8). (3) Anamwita Mwana, Mungu. Anatangaza kwamba ufalme wa Kristo ni wa milele.

Sababu nyingine ya kujua kuwa Mwana ni Mungu wa milele Mwenyewe, ni kwamba yeye anaabudiwa. Isaya 42:8, Kutoka 20:3, na aya nyingi nyingine za Agano la Kale zinakataza tusimwabudu mwingine zaidi ya Yehova Mungu Mwenyewe—lakini tunaona katika aya nyingi kwamba Kristo akiabudiwa (mifano—Wafilipi 2:9-10, Matendo 7:59-60, Ufunuo 5:6-14), ambako kunaabudiwa mbingu pekee.

Sababu nyingine inayotufanya tujue kuwa Yeye ni Mungu ni kwamba kazi za Mungu zinaelezwa kufanywa na Yeye, Uumbaji (Yn. 1:3, Ebr. 1:2) Utunzaji wa ulimwengu (Kol. 1:17, Ebr. 1:2-3), kumtuma Roho wa Mungu (Yn 16:7) msamaha wa dhambi (Mdo. 5:30-31) na kutoa uzima wa milele (Yn 17:2-3) hii ni mifano machache tu ya kazi za kimbingu alizozifanya.

Alidhihirisha uweza wake juu ya asili, juu ya magonjwa, nguvu za mapepo, hata juu ya mauti, na katika matukio mawili, aliondoa utaji wa ubinadamu wake kwa kiasi. Katika mlima alikogeuka sura aliwaruhusu wanafunzi wake kuiona hali yake ya utukufu kama ilivyo, na wakati maaskari walipokuja kumkamata bustanini, aliwapiga wakaanguka chini aliposema.. “NI MIMI” (neno hili halipo katika tafsiri halisi za awali) (Yn 18:4-6). Kwa kweli alifanya kazi za Mungu.

Sababu nyingine inayotulisha kuwa Mwana ni Mungu ni kwamba Ana sifa za kiungu. Biblia inasema Yeye alikuwepo tangu mwanzo (Yn. 5:26), Umilele (Yn 1:2). Kujua Yote (Yn. 1:48), Kuwepo Kila Mahali (Mt. 18:20—ona kwamba alikuwa duniani, katika mwili na alitumia wakati uliopo, kuonyesha kwamba alikuwa na sifa hii ya uungu katika huduma yake hapa duniani, Kutokubadilika (Ebr. 13:8), Ukuu (Mt. 11:27), Uweza Wote (Mt. 28:18-20). Kuna kauli za nguvu kabisa juu ya Uungu wa Masihi katika Yeremia 23:5-6.

“…Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA NI HAKI YETU.”

Hapa tuna Yehova Mungu akizungumza kwa wazi, kama vile ni Masihi anaongea, na jina analompa Masihi ni Yehova –Tsidkenu—Mungu Mwenyezi anamwita Masihi Yehova!

Roho Mtakatifu Ni Mungu

(Maelezo mengi ya sehemu hii yanatoka katika kitabu kizuri kiitwacho The Holy Spirit Kilichoandikwa na A.W. Pink.)

Katika kauli hii inachukuliwa kwamba Roho Mtakatifu ni Nafsi (Mtu), na sio nguvu, ushawishi n.k. Vikundi vya imani potofu huukataa uungu na utu wake. Anachukuliwa kama aina fulani ya “umeme wa mbinguni”, au aina fulani ya nguvu kutoka kwa Mungu ambayo nzuri duniani. Hii inaenda sambamba na kuukataa Utatu. Hata hivyo, tukiangalia katika Biblia tunaona kwamba ana sifa anazoelezewa katika Maandiko—kama vile uelewa na maarifa (1 Kor 2:10-11), maamuzi (1 Kor 12:11), upendo (Rum 15:30), na huzuni (Efe 4:30). Zaidi ya hayo anaweza kudanganywa (Mdo. 5:3); Anaweza kujaribiwa, (Mdo 5:9). Pia tunaona matendo ya kibinafsi yakimwelezea katika Maandiko: Ananena (1 Tim 4:1, Ufu 2:7); Anafundisha (Luka 12:12, Yn 14:26); Huamuru (Mdo 13:2); na, Huombea (Rum 8:26).

Biblia hutumia wasifu binafsi kumwelezea—Anaitwa Mfariji (Yn. 14:16), Shahidi (Ebr. 10:15, Warumi 8:16), Mhesabu Haki na Mtakasaji (1 Kor 6:11).

Mwisho, katika sehemu nyingi kwenye Maandiko, maneno ya kibinafsi yanatumika kumwelezea (Yn. 14:26; Yn 16:7). Sio tu kwamba Roho Mtakatifu ni Mtu lakini pia Roho Mtakatifu ni Mungu, kama ambavyo Baba ni Mungu na Mwana ni Mungu, kwa namna fulani Mungu wa Kweli Mmoja lakini kwa namna kuu kibinadamu, ni nafsi ya kipekee katika Utatu.

Katika Biblia Roho Mtakatifu anaitwa ni Mungu (Mdo. 5:3-5; 1 Kor. 3:16—Linganisha 2 Kor 6:16). Roho Mtakatifu pia anaitwa Yehova—Ni Yehova aliyenena kupitia manabii (Lk 1:68-70) na Petro anasema ilikuwa ni Roho Mtakatifu (2 Pet 1:20, linganisha na 2 Sam 23:2-3 na Mdo 1:16). Ilikuwa ni Yehova ambaye Israeli walimwasi jangwani (Zab 78:4, 17-18), lakini Isaya anasema alikuwa ni Roho Mtakatifu (Isa 63:10). Katika Kumb. 32:12, Yehova aliwaongoza Israeli lakini katika Isaya 63:14, inasema ni Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza. Yehova alimtuma Isaya nabii (Isa. 6:6-8), lakini Paulo anasema (chini ya Upako wa Roho Mtakatifu) kwamba alikuwa ni Roho Mtakatifu aliyemtuma nabii (Mdo 28:25-26).

Katika sehemu zote za Maandiko Roho Mtakatifu anadhihirisha sifa za Mungu katika matendo yake, utakatifu mkubwa na mdogo (Rum. 1:4; linganisha Kut. 15:11), Umilele (Ebr 9:14), Kuwepo kila mahali (Zab 139:7), Kujua Mambo yote (1 Kor 2:10 – 11) Kuwa na Nguvu Zote (Lk. 1:35; Mika 3:8; Isa 40:28), Mwenyezi (Mt 4:1—Alimwongoza Yesu!) (Yn 3:8, 1 Kor 12:11; Mdo 13:2-4; 20:28). Mwisho, Roho Mtakatifu hufanya kazi za Mungu. Alifanya kazi za Uumbaji (Ayu 26:13; 33:4; Mwa 1:2), Hutuhudumia (Isa 40:13-15; Mdo 16:6-7), Uvuvio (2 Pet 1:20-21), Kumpaka Mafuta Mwokozi (Isa 61:1; Yn 3:34), Kumfufua Mwokozi (Rum 8:11).

Fundisho la Utatu linamfunua Mungu ambaye ni tofauti sana na “miungu” ya kipagani, lakini pia ni tofauti sana na Mungu wa kimila wa kiyahudi, Waislam, Ariani na miungu wengine walioshamiri leo. Kuna tofauti kubwa kati ya Ukristo na dini nyingine zinazopinga Utatu. Kwenye dini hizi mambo muhimu mawili yanakosekana, nayo ni: mahusiano na ukombozi.

1. Mahusiano—mungu pekee yaani “mungu” ambaye hawa watu wanamwabudu huwa hawezi kufanya mahusiano. Hana wa kuhusiana naye, na wala hakuna jinsi ya kumfanya ahusiane na watu isipokuwa tu akiwa kama hakimu na akiwa kama kitu tu cha kuabudiwa. Mungu wa Utatu kwa upande mwingine ana ushirika ndani yake mwenyewe milele—na hutokea ndani yake. Kupitia Mungu-mwanadamu, Kristo Yesu, mtu huingia katika ushirika na mahusiano na Mungu Mwenyezi. Baba ni Baba yetu; Kristo ni Kaka yetu, na Roho ni Mfariji wetu. Tunapendwa, tunatembea katika ushirika na Mungu, ambaye ni mtaalam wa ushirika wa kweli.

2. Ukombozi—Dini zinazoukataa Utatu hazina ukombozi halisi. Mungu wao husamehe au kutoa rehema bila utaratibu unaoeleweka. Huhukumu au kuachilia kulingana na hali yake ya kujisikia, kwa kutumia masharti fulani-fulani. Dhambi haishughulikiwi kwa uhalisia wake, mtu hawajibishwi na huyo mungu wao anaweza tu kuipuuza. Hakuna haki kwenye mfumo wa aina hii. Katika Ukristo wa Kibiblia, kila dhambi inalipiwa, kwa sababu Mungu wa milele, Mungu-mwanadamu alikufa kuwalipia wenye dhambi. Wote wanaokuwa Wake kwa imani wanakuwa washiriki katika bei yake ya ukombozi.Wale ambao hawawi wake wanalipia adhabu yao—milele. Siri ya Msalaba ni kwamba Mungu-Baba alimwaga ghadhabu yake kwa Mungu-Mwana, lakini ni Mungu mmoja tu. Hili linachanganya akili zetu lakini hivyo ndivyo namna ya pekee ukombozi ungeweza kufanyika kwa haki. Kila kosa ambalo liliwahi kutendeka na mtu yeyote dhidi ya Mungu au watu linaadhibiwa, haki inatendeka na hali ya ulimwengu inawekwa sawa. Kama hakuna Utatu—hakuna ukombozi.

Sisi Wakristo tunamwabudu Mungu wa Utatu. Hatuwezi kuelewa; tunaushangaa; hakuna maelezo—lakini huo ndio Ukweli. Kikipungua chochote hapo basi sio Ukristo.

Mafundisho haya yametolewa na Charles T. Buntin na kutafsiriwa na Emmanuel A. Lyatuu

Charles T. Buntin ni Mwanajeshi Mstaafu ambaye ni Mtumishi wa Kanisa la Baptist Marekani.

Yeye pia ni mwalimu wa masomo ya Sanaa katika Sekondari.

Ana Shahada ya B.A katika Historia, M.S. Katika Uhusiano wa Kimataifa na M.A.R. kutoka Liberty University.

Kwa sasa anafanya kazi kama Mhadhiri na Mnasihi katika chuo cha Trinity Seminary kilichoko Newburgh, Indiana Marekani na pia anafanya shughuli za unasihi wa Kibiblia katika huduma iitwayo Covenant Counseling Ministries

Related Topics: Basics for Christians, Trinity

Report Inappropriate Ad